Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya Salum, amesema siyo haramu kwa Watanzania kuweka fedha nje hivyo,
Watanzania 99 waliotajwa kuwa na akaunti Uswisi haimaanishi wote wametorosha
fedha.
Hata hivyo,
amsema serikali inaangalia ripoti ya Swiss Leaks ili kuona uhalali wa akaunti
hizo za siri.
“Sisi hatujaona
kama ni kosa kwa Watanzania kuwekeza fedha zao kwenye mabenki ya nje na wala
isionekane kama ni jambo haramu kabisa.
Kama serikali
tungetamani wawekeze kwenye benki nchini ili kukuza sekta ya fedha lakini pia
hatuwafungi kutowekeza nje,” alisema.
“Tunachofanya ni
kuiangalia hiyo ripoti ili kujua ukweli wa taarifa hizo, lakini taarifa hiyo
haimaanishi kwamba ni kosa kubwa kisheria kwa Mtanzania kuweka fedha nje,”
alisema.
Mkuya alisisitiza
kuwa hakuna shida yoyote kwa Watanzania kuweka fedha kwenye akaunti nje ya
nchi.
Waziri Mkuya
ameyasema hayo siku moja tu baada ya vyombo vya habari nchini kuripoti taarifa
ya kuwapo vigogo 99 wa Tanzania kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za
Uswisi kutokana na ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa
Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ).
Taarifa ya Swiss
Leaks iliyotolewa juzi Jumapili, inaonyesha kuwa vigogo hao wa Tanzania wana
akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114 ambazo ni sawa na Sh.
bilioni 199.6.
Msingi wa ripoti
hiyo umetokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC, Hervé
Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha kazi; na mwaka
2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi wa umma na
wanasiasa kwa Serikali ya Ufaransa ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya
uchunguzi na kuthibitisha.
Ripoti hiyo ya Swiss Leaks, inaeleza kuwa taarifa za kiuchunguzi
kutoka benki ya HSBC nchini Uswisi zinaonyesha kuwa akaunti hizo
zinahusishwa na baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na watumishi wa
umma ambao wamejipatia utajiri wa siri unaotokana na kampuni hewa (offshore
companies)