Mkutano
Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) utafanyika Novemba 15 mwaka huu jijini
Dar es Salaam ambapo moja ya ajenda ni uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi moja ya
uongozi kwenye bodi hiyo.
Nafasi
hiyo ya ujumbe kwenye Kamati ya Uendeshaji ya TPLB iliyokuwa ikishikiliwa na Kazimoto
Muzo imebaki wazi baada ya klabu yake ya Pamba ya Mwanza kushuka daraja kutoka
la Kwanza hadi la Pili.
Hivyo,
wagombea wa nafasi hiyo ni kutoka kwenye klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Klabu hizo zina nafasi mbili kwenye Kamati ya Uendeshaji ya TPLB ambapo
nyingine inashikiliwa na Omari Mwindadi wa klabu ya Mwadui ya Shinyanga.
SDL WAONGEZEWA
MUDA WA USAJILI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza muda wa usajili wa wachezaji kwa
timu za Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa siku saba ambapo sasa utamalizika Oktoba
21 mwaka huu.
Awali
usajili huo unaofanyika kwa njia ya mtandao (online) ulikuwa umalizike jana
(Oktoba 14 mwaka huu), lakini ni klabu chache ndizo zilizoweza kusajili ndani
ya muda uliopangwa.
Klabu
ambazo hazijakamilisha shughuli hiyo ya usajili, zinatakuwa kukamilisha ndani
ya siku hizo saba kwani TFF haitaongeza tena muda wa usajili. Vilevile klabu za
SDL zinakumbushwa kuwasilisha majina ya viwanja vya nyumbani ambavyo timu zao
zitatumia kwenye ligi hiyo.
TFF
ilifanya mafunzo ya usajili kwa maofisa usajili wa klabu hizo Oktoba 6 na 7
mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Timu
za SDL zimegawanywa katika makundi manne ya timu sita zitakazocheza ligi kwa
mtindo wa nyumbani na ugenini. Kundi A lina timu za Mpanda United ya Katavi,
Ujenzi (Rukwa), Mvuvumwa FC (Kigoma), Mji Mkuu FC (Dodoma), Milambo (Tabora) na
Singida United (Singida).
Kundi
B ni Mbao FC (Mwanza), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), JKT
Rwamkoma (Mara), Pamba (Mwanza) na AFC (Arusha). Kundi C ni Navy, Mshikamano,
Transit Camp na Abajalo za Dar es Salaam, Kiluvya United (Pwani) na Kariakoo
(Lindi(.
Timu
zinazounda kundi D ni Magereza (Iringa), Town Small Boys (Ruvuma), Njombe Mji
(Njombe), Volcano FC (Morogoro), Wenda FC (Mbeya) na Mkamba Rangers (Morogoro).
MAREKEBISHO
YA RATIBA FDL KUNDI A
Mechi nne za Kundi
A la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zimefanyiwa marekebisho ili kutoa fursa ya
matumizi ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Timu za
African Lyon na Kimondo FC ambazo awali zilikuwa zicheze Oktoba 25 mwaka huu
kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, sasa zitacheza Oktoba 26 mwaka huu
Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Nayo mechi ya
Polisi Dar es Salaam na Majimaji ya Songea iliyokuwa ichezwe Oktoba 26 mwaka
huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, sasa itachezwa Oktoba 27 mwaka huu kwenye
uwanja huo huo.
Mechi ya
Friends Rangers na Ashanti United iliyokuwa ichezwe Mabatini mkoani Pwani,
Oktoba 26 mwaka huu, sasa itachezwa Uwanja wa Karume, Oktoba 28 mwaka huu.
Pia mechi ya
Lipuli FC na JKT Mlale iliyokuwa ichezwe Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa
Samora mjini Iringa, imesogezwa mbele kwa siku moja. Mechi hiyo sasa itachezwa
Oktoba 26 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
No comments:
Post a Comment