pichani ni Waziri wa Afya Dokta Seif Rashid |
MFUKO wa Bima ya Afya (NHIF), umekumbwa
na kashfa ya ufisadi ya kutumia zaidi ya sh. milioni 200 kununua gari
jipya ambalo wamemkabidhi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif
Rashid.
Pia Bodi ya mfuko huo ambayo hupata
fedha kutokana na michango ya wanachama wake, imetumia zaidi ya sh.
bilioni mbili katika kipindi kisichozidi miezi sita badala ya mwaka
mzima kama ilivyotengewa kwenye bajeti ya mfuko huo kwa mwaka huu wa
fedha.
pichani ni Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Khamis Mdee, |
Uchunguzi wa Chanzo chetu, umebaini kuwa gari hilo lilinunuliwa kwa ajili ya matumizi ya Mkurugenzi wa Mfuko huo.
Gari hilo aina ya Nissan toleo jipya
kabisa, lenye namba za usajili SU 39931, lilikabidhiwa kwa Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Rashid Oktoba 11, mwaka huu, saa 9.15 na
sasa limebadilishwa namba na kuwekwa kibao cha Waziri wa Afya (W AF).
Sababu inayotajwa na NHIF kukabidhi gari
hilo kwa waziri huyo ni kwamba gari lake la awali alilopewa na serikali
wakati anaingia wizarani, limeharibika na liko kwenye matengenezo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya mfuko
huo, vililiambia Chanzo kuwa uamuzi wa kulikabidhi gari hilo kwa
waziri, ulitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Khamis Mdee ambaye
aliwaagiza wafanyakazi wa idara ya rasilimali watu kutekeleza agizo hilo
na hakutaka kuulizwa maswali.
Baadhi ya watumishi wa mfuko huo
walienda mbali zaidi wakidai kuwa Mdee alitoa gari hilo kwa waziri kama
moja ya ushawishi wa kutaka ateuliwe kuwa mkurugenzi mpya wa mfuko,
kushika nafasi iliyoachwa wazi na Emmanuel Humba aliyemaliza muda wake.
“Kwa kawaida mawaziri hupewa magari na
serikali na hata yakiharibika matengenezo yake yanagharimiwa na
serikali, lakini sio kazi ya taasisi yoyote ya umma iliyo chini ya
wizara husika kununua gari kwa ajili ya waziri.
“Hivi leo kaimu mkurugenzi wetu akikosea
kitu chochote kile, waziri aliyepewa gari hilo atakuwa na uwezo wa
kumwajibisha?”alihoji mmoja wa maafisa waandamizi wa mfuko huo ambaye
aliomba jina lake lihifadhiwe.
Bodi yatafuna bil.2/-
Kuhusu kashfa ya matumizi ya sh. bilioni
2 katika kipindi kisichozidi miezi sita, uchunguzi umebaini kuwa feha
hizo zilitengwa kwa ajili ya bajeti ya Bodi ya wakurugenzi kwa mwaka huu
wa fedha.
“Jambo la ajabu ni kwamba, bodi hiyo
imetumia fedha hizo ndani ya miezi mitatu tu na sasa inaishi kwa kukopa
kutoka kwenye kasma zingine,” alisema mtoa taarifa wetu.
Habari zinasema kuwa bodi hiyo imekuwa
ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kufanya ziara za mafunzo nje ya nchi
na zimekuwa zikigharimua mamilioni ya fedha.
Mkuregenzi ajitetea
Kaimu mkurugenzi wa NHIF, Mdee
alipoulizwa kuhusu madai hayo, alikiri taasisi yake kukabidhi gari hilo
kwa waziri wa Afya, lakini alikana kwamba hatua hiyo haina nia ya
kushawishi ateuliwe kuwa mkurugenzi mpya wa mfuko huo.
Akizungumza na Chanzo chetu, alisema huo ni utaratibu wa kawaida na hata utoaji wa gari hilo umezingatia matakwa ya sheria.
Alisema mfuko huo umeamua kukabidhi gari
hilo kwa waziri huyo kwani gari lake la awali alilokuwa akilitumia
limeharibika na litakapotengamaa gari hilo litarudishwa mikononi mwa
NHIF.
“Tuhuma hizo na nyingine zote
unazozisikia ni majungu ambayo sijui lengo lake. Huyo ni waziri wetu na
taasisi hii ipo chini ya wizara yake. Kuna ubaya gani kumpa gari
akalitumia kwa muda wakati anasubiri gari lake?” alihoji Mdee na
kusisitiza kuwa hayo ni majungu.
Akijibu madai kwamba ametoa gari hilo
kama ushawishi wa kutaka uteuzi wa ukurugenzi, Mdee alisema wenye
mamlaka ya uteuzi huo wako juu na hakuna namna mtu anaweza kufanya
ushawizi ili ateuliwe.
Baada ya Humba aliyeasisi kuanzishwa kwa
mfuko huo, kumaliza muda wake, Bodi ya wakurugenzi ilimteua Mdee
kukaimu nafasi ya hiyo.
Serikali ilitangaza nafasi hiyo kuwa
wazi na kuwataka wenye sifa kuomba, lakini hadi sasa mchakato wa kumpata
mkurugenzi mpya, bado unaendelea. Hata hivyo ni miezi sita sasa imepita
tangu kukamilika kwa usaili wa kumtafuta mkurugenzi mkuu mwingine na
Mdee anapewa nafasi kubwa.
Kauli ya Wizara
Akizungumza na Chanzo chetu, Msemaji wa
Wizara ya Ujenzi ambayo pamoja na mambo mengine inahusika na suala la
magari ya viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri, Segolema Francis
alisema hawana taarifa na gari la Waziri wa Afya kuharibika na pia
hawana taarifa kama Bima ya Afya kutoa gari kwa ajili ya kumsaidia
waziri katika kipindi hiki.
“Kweli tunahusika na magari ya mawaziri
na watendaji wengine wa serikali, lakini hatujui kama waziri unayemtaja
hana gani na ameazimwa la NHIF. Naomba unipe muda nifuatilia suala hilo
hadi leo tunalitolea majibu,” alisema.
No comments:
Post a Comment