Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linakaribisha
wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani
na ugenini. Ubunifu ni lazima uzingatie rangi za bendera ya Taifa.
Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata sh. 1,000,000 (milioni moja),
na mshindi wa jezi ya ugenini atapata pia sh. 1,000,000 (milioni moja).
Ubunifu utumwe kwenye anwani ya barua pepe: info@tff.or.tz
au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF
zilizopo ghorofa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden
Avenue. Mwisho wa kupokea designs ni Novemba 15, 2014.
Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi kwa simu namba; 0713
210242 au 0714 634838.
SDL KUANZA
KUTIMUA VUMBI NOVEMBA 22
Michuano ya Ligi
Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 zitakazocheza katika makundi manne
ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza kutimua vumbi
Novemba 22 mwaka huu.
Kamati ya
Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyoketi jijini Dar
es Salaam jana (Oktoba 29 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange ilipitia
maandalizi maandalizi ya ligi hiyo ikiwemo mwongozo wake (roadmap).
Kwa mujibu wa
mwongozo huo, usajili wa wachezaji utamalizika Oktoba 31 mwaka huu. Kipindi cha
pingamizi ni kuanzia Novemba 1 hadi 7 mwaka huu wakati Kamati ya Sheria na
Hadhi za Wachezaji inatarajia kukutana Novemba 11 mwaka huu kwa ajili ya
kupitisha usajili.
Pia Kamati ya
Mashindano imepitisha viwanja vya timu zote, isipokuwa uwanja wa timu ya Mpanda
United ya Katavi na ule wa Town Small Boys ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Uwanja wa Town
Small Boys haukupitishwa kwa vile hauna uzio wa kudumu ( wa chuma) wa
kutenganisha wachezaji na washabiki, na pia ufikaji wa timu Tunduru ni mgumu
kutokana na ubovu wa barabara ikizingatiwa kuwa ligi hiyo itachezwa hadi
kipindi cha Masika.
Kwa upande wa
uwanja wa Mpanda United, umekataliwa kwa vile hauna vigezo vya msingi
vinavyotakiwa ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo, kutokuwa na nyasi na uzio
wa kudumu kutenganisha wachezaji na washabiki.
Kutokana na
uamuzi huo, Mpanda United sasa itatumia Uwanja wa Mandela uliopo Sumbawanga
wakati Town Small Boys itachezea mechi zake kwenye Uwanja wa Majimaji mjini
Songea.
29 WAITWA KIKOSI CHA MABORESHO
TAIFA STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatarajia
kuendelea na awamu ya pili ya maboresho ya timu ya Taifa (Taifa Stars)
inayojumuisha vijana wenye umri chini ya miaka miaka 23.
Katika awamu hii, Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij ameteua
majina ya wachezaji 29 ambao watakuwa wakiingia kambini mara moja kwa mwezi
siku ya Jumapili baada ya kuwakilisha timu zao kwenye mechi za ligi.
Kikosi hicho cha maboresho kitakuwa kikifanya programu
maalumu za mazoezi mpaka siku ya Jumatano na kucheza mechi za kirafiki na timu
za ndani au nje ya nchi.
Lengo hasa la programu hiyo ni kuwajengea uwezo vijana wenye
vipaji ambao walipatikana katika awamu ya kwanza ya mpango wa maboresho
mwanzoni mwa mwaka huu Tukuyu mkoani Mbeya, lakini wamekuwa hawatumiki. Pia
kuwandaa vijana ili kujenga timu ya ushindani na imara ya Taifa ya muda mrefu.
TFF ina imani kubwa kuwa programu hii itakuwa na manufaa kwa
soka ya Tanzania. Timu
hiyo itaingia kambini kwa mara ya kwanza Desemba 9 mwaka huu katika hoteli
itakayotangazwa baadaye.
Wachezaji walioteuliwa ni Aishi manula (Azam), Benedict
Tinoco (Kagera Sugar), Aboubakar Ally (Coastal Union), Miraji Adam (Simba),
Andrew Vicent (Mtibwa Sugar), Gadiel Mbaga (Azam), Emmanuel Semwanda (African
Lyon) na Joram Mgeveke (Simba).
Edward Charles (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Kassim
Simbaulanga (African Lyon), Pato Ngonyani (Yanga), Adam Salamba (Kahama),
Hassan Banda (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Hashim Magoma (Stand United),
Makarani Ally (Mtibwa Sugar), Said Juma (Yanga) na Said Hamis (Simba).
Aboubakary Ally Mohamed (Zanzibar), Hassan Dilunga (Yanga),
Hussein Malombe (Geita Gold), Muzamir Ally (Mtibwa Sugar), Shiza Ramadhan
(Mtibwa Sugar), Omari Nyenje (Ndanda SC), Kelvin Friday (Azam), Salim Mbonde
(Mtibwa Sugar), Alfred Masumbakenda (Kahama) na Simon Msuva (Yanga).
IMETOLEWA
NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment