Wakati raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inakamilika leo
(Desemba 29 mwaka huu) kwa mechi tatu, ligi hiyo itaingia raundi ya tisa
Januari 3 mwakani kwa mechi tano.
Coastal Union itacheza na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani,
Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam
itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Stand United
itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na
Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Sokoine.
Ligi hiyo ambayo itachezwa mfululizo (non-stop) hadi
itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha raundi ya tisa Januari 4 mwakani
kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na
Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.
Nayo mechi kati ya Mtibwa Sugar na Stand United ambayo jana
ilivunjwa na mvua dakika ya 6 imemaliziwa leo ambapo timu hizo zimetoka sare ya
bao 1-1.
Wakati huo huo, mechi ya ligi iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja
wa Azam Complex imemalizika kwa wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao
1-0 dhidi ya JKT Ruvu. Bao hilo lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa
penalti uliopigwa na Hamisi Kasanga.
MBAO
FC YAKAMATA USUKANI SDL
Timu ya Mbao FC ya Mwanza imekamata uongozi wa Kundi B la michuano
ya Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha
JKT Rwamkoma ya Mara mabao 2-1.
Kwa matokeo hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM
Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa
kwa kushinda mechi zote tatu dhidi ya Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma.
Mbao FC inafuatiwa na JKT Rwamkoma yenye pointi sita, Arusha FC
pointi sita wakati Bulyanhulu na Pamba zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila
moja. Kundi hilo litakamilisha mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi
kati ya JKT Rwamkoma na Arusha FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.
Katika kundi A, Mji Mkuu (CDA) na Singida United ndizo
zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba kila moja. Timu hizo
zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa FC yenye pointi moja wakati
Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina pointi.
Hata hivyo, Mvuvumwa FC na Milambo ziko nyuma kwa mechi moja.
Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu kati ya timu hizo itachezwa kesho
(Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Kiluvya United imeendelea kuchachafya kundi C baada ya kushinda
mechi zote ne ilizocheza, hivyo kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano
yenye pointi saba huku Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.
Nafasi ya nne inashikwa na Transit Camp yenye pointi nne,
Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano wakati Kariakoo ambayo haina pointi
ni ya mwisho. Hata hivyo, Cosmopolitan na Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.
Mechi zinazofuata za kundi hilo ni Januari 3 mwakani kati ya
Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano (Ilulu), Transit Camp na Abajalo
(Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya (Karume).
Kundi D, vinara bado ni Njombe Mji yenye pointi 12 ikifuatiwa na
Wenda yenye pointi sita wakati Volcano FC iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi
tano. Mkamba Rangers ina pointi nne, Town Small Boys ina pointi moja wakati
Magereza FC haina pointi.
Katika kundi hilo leo (Desemba 28 mwaka huu) kutakuwa na mechi
kati ya Town Small Boys na Magereza itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini
Songea. Januari 3 mwakani kutakuwa na
mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na Magereza, na Wenda
na Mkamba Rangers.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)