Monday, 29 December 2014

LIGI KUU YA VODACOM YAINGIA RAUNDI YA 9


Wakati raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inakamilika leo (Desemba 29 mwaka huu) kwa mechi tatu, ligi hiyo itaingia raundi ya tisa Januari 3 mwakani kwa mechi tano.

Coastal Union itacheza na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ligi hiyo ambayo itachezwa mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.

Nayo mechi kati ya Mtibwa Sugar na Stand United ambayo jana ilivunjwa na mvua dakika ya 6 imemaliziwa leo ambapo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.

Wakati huo huo, mechi ya ligi iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex imemalizika kwa wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu. Bao hilo lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Hamisi Kasanga.  

MBAO FC YAKAMATA USUKANI SDL
Timu ya Mbao FC ya Mwanza imekamata uongozi wa Kundi B la michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha JKT Rwamkoma ya Mara mabao 2-1.

Kwa matokeo hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa kwa kushinda mechi zote tatu dhidi ya Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma.

Mbao FC inafuatiwa na JKT Rwamkoma yenye pointi sita, Arusha FC pointi sita wakati Bulyanhulu na Pamba zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila moja. Kundi hilo litakamilisha mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi kati ya JKT Rwamkoma na Arusha FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.

Katika kundi A, Mji Mkuu (CDA) na Singida United ndizo zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba kila moja. Timu hizo zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa FC yenye pointi moja wakati Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina pointi.

Hata hivyo, Mvuvumwa FC na Milambo ziko nyuma kwa mechi moja. Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu kati ya timu hizo itachezwa kesho (Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Kiluvya United imeendelea kuchachafya kundi C baada ya kushinda mechi zote ne ilizocheza, hivyo kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano yenye pointi saba huku Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.

Nafasi ya nne inashikwa na Transit Camp yenye pointi nne, Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano wakati Kariakoo ambayo haina pointi ni ya mwisho. Hata hivyo, Cosmopolitan na Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.

Mechi zinazofuata za kundi hilo ni Januari 3 mwakani kati ya Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano (Ilulu), Transit Camp na Abajalo (Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya (Karume).

Kundi D, vinara bado ni Njombe Mji yenye pointi 12 ikifuatiwa na Wenda yenye pointi sita wakati Volcano FC iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano. Mkamba Rangers ina pointi nne, Town Small Boys ina pointi moja wakati Magereza FC haina pointi.

Katika kundi hilo leo (Desemba 28 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Magereza itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.  Januari 3 mwakani kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na Magereza, na Wenda na Mkamba Rangers.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment