Tuesday, 19 August 2014

MTIBWA, POLISI MORO KUCHEZA MECHI YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI


Timu za Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro zinazojiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitacheza Jumamosi (Agosti 23 mwaka huu) mechi ya majaribio ya mfumo wa tiketi za elektroniki.

Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kuanzia saa 10 jioni wakati kiingilio kitakuwa sh. 1,000.

Tiketi za mechi hiyo zitaanza kuuzwa kesho (Agosti 20 mwaka huu) kupitia mtandao wa M-Pesa, CRDB Simbanking na maduka 30 ya Fahari Huduma yaliyopo katika wilaya zote za Mkoa wa Morogoro, wengi wao wakiwa Morogoro Mjini.

Washabiki 100 wa kwanza kuingia uwanjani wapata jezi za timu za Mtibwa Sugar na Polisi.

Tayari mechi ya majaribio ya tiketi za elektroniki imeshafanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo timu za Tanzania Prisons na Mbeya City zilipambana na kutoka sare.

Mechi nyingine za majaribio ya tiketi za elektroniki zitachezwa Agosti 30 mwaka huu. Uwanja wa Mkwakwani jijini utakuwa na mechi kati ya Coastal Union na Mgambo Shooting wakati katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ni Kagera Sugar dhidi ya mabingwa wa Mkoa wa Kagera, Eleven Stars.

Septemba 6 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa kutakuwa na mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar. Mechi nyingine ni ya Ngao ya Jamii kati ya Azam na Yanga itakayofanyika Septemba 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

WAAMUZI KUFANYA MTIHANI WA UTIMAMU WA MWILI

Waamuzi wanaotarajia kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu watafanya mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) mwezi ujao.

Mtihani huo utahusisha waamuzi wa daraja la kwanza (class one) wakiwemo pia wale wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mbali ya mtihani huo unaotarajiwa kufanyika kabla ya Septemba 10 mwaka huu, pia kutakuwa na semina kwa makamishna ambao watasimamia mechi za VPL na FDL.

Hivyo waamuzi wote wanatakiwa kutumia muda uliobaki kufanya maandalizi kwa ajili ya mtihani huo.

No comments:

Post a Comment