Makamu Mwenyekiti wa TAHLISO Abdi Mahmoud Abdi akizungumza
na Waandishi wa habari leo Mjini Idara ya Habari maelezo Zanzibar
kuhusu kukanusha Taarifa ya Maandamano yaliyopangwa kufanyika hapo
kesho.
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 14/08/2014
Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo
Vikuu TAHLISO limekanusha Taarifa zilizosambazwa katika Vyombo vya
habari na Mitandao ya Kijamii juu ya kuwepo wa maandamano ya Wanafunzi
wa Vyuo vikuu yanayotarajiwa kufanyika hapo kesho Ijumaa.
Shirikisho hilo pia limesema
Taarifa za kuwepo kwa maandamano hayo hazijatolewa na TAHLISO na
kuwaomba Wanafunzi kutojaribu kushiriki katika Maandamano hayo.
Akizungumza na Waandishi wa habari
leo Mjini Zanzibar Makamu Mwenyekiti wa TAHLISO Abdi Mahmoud Abdi
amesema aliyesambaza Taarifa za Maandamano hayo ni Mtu ambaye
alishavuliwa Nyadhifa za Uongozi wa TAHLISO na kwamba anachokifanya ni
Upotoshaji na kujipalilia kisiasa.
“Anayejiita Mwenyekiti wa TAHLISO
Musa Mdede SI MWENYEKITI HALALI kwasababu vikao halali vya Shirikisho
vilivyofanyika May 3,4,2014 katika Chuo cha kodi vilimwondoa madarakani
na kwa mujibu wa Katiba nafasi yake ilikaimiwa na Makamu wake ” Alisema
Abdi
Amesema sababu ya Msingi ya
kumuondoa katika nafasi yake ilitokana na kwenda kinyume na Katiba kwa
kujiingiza katika Siasa ambapo aligombea na kuangushwa katika kura za
maoni kupitia CHADEMA.
Amedai kuwa anachokifanya Mdede
kwa sasa ni upotoshaji kwa TAHLISO ambapo anajitangaza kwa malengo ya
kugombea uchaguzi mkuu unaokuja wa mwaka 2015.
Amefahamisha kuwa licha ya kuwepo
na Taarifa ya Baadhi ya Vyuo kutokupata Pesa kwa ajili ya Mafunzo ya
Vitendo TAHLISO imekuwa bega kwa bega kuhakikisha suala hilo linapatiwa
majibu ya haraka.
Amesema BODI ya Mikopo inaendelea
kuchukua hatua za haraka katika kuhakikisha Vyuo husika Vinapatiwa fedha
na kwamba siku ya Leo Bodi itatoa Fedha kwa Chuo kikuu Kishiriki cha
kumbukumbu ya Stephano Moshi (SMUCCO) na Chuo kikuu cha Jordan
Morogoro.
“Chuoni siyo sehemu ya kufanya
Siasa bali ni sehemu ya kusoma, Maandamano siyo suluhu njia pekee ni
mazungumzo na tunaendelea kuyafanya” Alifafanua Abdi.
Aidha Makamu Abdi amesema taratibu
zinazohitajika zinaendelea kuchukuliwa ili Vyuo vingine vilivyobakia
viweze kupata fedha hizo.
Vyuo ambavyo havijapata Fedha za
Mafunzo kwa Vitendo ni pamoja na Chuo kikuu cha Mtakatifu
Augustino(SAUT) Mwanza na Tabora, Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM), Chuo
kikuu cha Teofilo Kisanji Mbeya na Chuo kikuu cha Tumaini
Makumira-Iringa.
Katika taarifa zilizosambaa kwenye
Vyombo vya habari na Mitandao ya kijamii inadaiwa kesho Ijumaa
kutafanyika Maandamano ya amani ya Wanafunzi wa Vyuo vikuu kuelekea
Ofisi za Waziri Mkuu kushinikiza Serikali kutoa Shiligi Bilioni 6.6 kwa
ajili ya mafunzo ya Vitendo kwa wanafunzi hao.
Makamu huyo ambaye anashika nafasi
ya Uenyekiti kwa sasa amewaomba Wanafunzi ambao hawajapata fedha zao
kuwa watulivu wakati wakisubiri kupata fedha zao huku hatua za haraka
zikichukuliwa.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment