Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) litatuma waangalizi wa siri kwenye mechi za raundi ya 21 na 22 ambazo ni
za mwisho kwa makundi yote ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakazoanza
kuchezwa Februari 10 mwaka huu.
Mwangalizi huyo (match assessor)
atatumwa na Katibu Mkuu ambapo baada ya mechi atatuma ripoti kwake kwa hatua
zaidi.
Mechi za raundi ya 21 kundi A zitachezwa
Februari 10 mwaka huu kati ya KMC na African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani),
Kurugenzi FC na African Sports (Uwanja wa Mufindi), Majimaji na JKT Mlale
(Uwanja wa Majimaji), Kimondo FC na Friends Rangers (CCM Vwawa, Mbozi), Ashanti
United na Villa Squad (Uwanja wa Karume) na Polisi Dar na Lipuli FC (Uwanja wa
Azam Complex).
Raundi ya 22 itachezwa Februari 16 mwaka
huu kwa kuzikutanisha African Lyon na Polisi Dar (Uwanja wa Karume), Kurugenzi
na Lipuli FC (Uwanja wa Mufindi), Kimondo FC na Majimaji (CCM Vwawa, Mbozi),
JKT Mlale na Ashanti United (Uwanja wa Majimaji), Friends Rangers na African
Sports (Uwanja wa Taifa), na Villa Squad na KMC (Uwanja wa Azam Complex).
Kundi B raundi ya 21 ni Februari 17
mwaka huu kati ya Burkina Faso na JKT Kanembwa (Uwanja wa Jamhuri), Mwadui na
Polisi Tabora (Uwanja wa Mwadui), Polisi Dodoma na Green Warriors (Uwanja wa
Jamhuri), Rhino Rangers na JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Panone na Polisi
Mara (Uwanja wa Ushirika), Geita Gold na Toto Africans FC (Geita).
Februari 22 mwaka huu ni JKT Kanembwa na
Green Warriors (Lake Tanganyika), Mwadui na Burkina Faso (Mwadui), Polisi
Tabora na JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Polisi Dodoma na Panone (Uwanja wa
Jamhuri), Toto Africans na Rhino Rangers (CCM Kirumba) na Geita Gold na Polisi
Mara (Geita).
Mechi za viporo za Polisi Mara
zitachezwa Februri Mosi dhidi ya JKT Kanembwa, na Februari 5 mwaka huu dhidi ya
Polisi Tabora. Mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.
FIFA YACHUNGUZA TUHUMA ZA UPANGAJI
MATOKEO
Ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) upo nchini kuchunguza tuhuma za upangaji matokeo.
Waamuzi waliosimamishwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) pamoja na watu wengine
watahojiwa na ujumbe huo. Matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa na FIFA baada
ya shughuli hiyo kukamilika.
Tunaendelea kuwahimiza wanafamilia wa mpira wa
miguu wazidi kuzingatia kanuni za maadili za TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) na FIFA katika utendaji wao. FIFA itahakikisha kuwa haki
inatendeka katika uchunguzi ambao inaufanya.
TFF YAHADHARISHA MGOGORO WA ZFA KORTINI
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)l imepokea kwa masikitiko taarifa za kuwepo tena kortini
kwa kesi dhidi ya uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), jambo
ambalo linaweza kuathiri ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye Ligi ya Mabingwa
Afrika, na Kombe la Shirikisho.
Mwishoni mwa mwaka jana,
TFF ilihadharisha juu ya masuala ya mpira wa miguu kupelekwa mahakamani, kwani kwa
mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kitendo hicho ni
kinyume cha taratibu za uendeshaji mpira wa miguu ambazo zinakataza masuala ya
mchezo huo kupelekwa katika mahakama za kawaida.
Kutokana na hali hiyo,
TFF iliiandikia barua ZFA kutaka mgogoro huo uondolewe kortini na yenyewe kuridhia
kuwa tayari kupeleka ujumbe Zanzibar ili ukutane na pande zinazohusika.
Pia TFF ilisema timu za
Tanzania Bara zisingeruhusiwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015
iwapo kesi hiyo ingeendelea kuwepo kortini na kutaka iondolewe bila masharti
yoyote.
ZFA iliithibitishia TFF
kuwa kesi hiyo imeondolewa kortini bila masharti, hivyo timu za Tanzania Bara
kuruhusiwa kushiriki katika michuano ya Kombe la Mapinduzi. Ni muhimu suala hilo likashughulikiwa haraka ili
kutohatarisha ushiriki wa timu za KMKM na Polisi kwenye michuano hiyo ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)