Monday, 26 January 2015

FDL KUSIMAMA KUPISHA VIPORO VYA POLISI MARA


Mechi za raundi ya 20, 21 na 22 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote zimesimamishwa ili kupisha Polisi Mara imalize mechi zake za viporo, na timu zote zicheze mechi zao za raundi zilizobaki kwa pamoja.

Polisi Mara ilifungiwa kutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma kutokana na vurugu zilizojitokeza kwenye mechi zake, hivyo kusababisha kuwepo kwa mechi hizo za viporo dhidi ya JKT Kanembwa na Polisi Tabora.

Tayari Polisi Mara tumeiruhusu itumie tena Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kwa mechi zake za nyumbani baada ya kuipa onyo kali kutokana na vurugu hizo. Lakini pia mechi zake kwenye uwanja huo zitachezwa chini ya uangalizi.

Uamuzi wa kupisha Polisi Mara imalize mechi zake za viporo una lengo la kuhakikisha mechi zote za raundi tatu za mwisho zinachezwa pamoja ili kuepuka uwezekano wa kupanga matokeo.

Pia klabu za FDL zenyewe ziliwasilisha ombi la kutaka mechi hizo za mwisho zichezwe kwa wakati mmoja.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) wakati wowote kuanzia kesho (Januari 27 mwaka huu) itatoa ratiba ya mechi za viporo za Polisi Mara, pamoja na tarehe mpya za mechi za raundi ya 20, 21 na 22.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment