Friday, 23 January 2015

6 ZAFUZU ROBO FAINALI KOMBE LA TAIFA WANAWAKE


Timu za mikoa sita tayari imepata tiketi za kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake itakayoanza Januari 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati nyingine mbili zinajulikana leo (Januari 23 mwaka huu).

Mikoa ambayo timu zake tayari zina tiketi za robo fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin ni Ilala, Kigoma, Mwanza, Pwani, Tanga na Temeke.

Matokeo ya mechi za leo kati ya Iringa na Ruvuma, na ile kati ya Mbeya na Katavi ndiyo yatakayoamua ni timu zipi mbili kati ya hizo zinakwenda Dar es Salaam kucheza robo fainali.

Timu zote zilizofuzu hatua ya robo fainali zinatakiwa kuripoti Dar es Salaam keshokutwa (Januari 25 mwaka huu). Fainali ya michuano hiyo itachezwa Februari Mosi mwaka huu.

TIMU YA BEACH SOCCER ZANZBAR YAWASILI DAR
Timu ya beach soccer ya Zanzibar imewasili Dar es Salaam leo mchana, tayari kwa kambi ya pamoja na Tanzania Bara kwa ajili ya kuunda kikosi cha Tanzania kitakashiriki mechi za mchujo za michuano ya Afrika.

Tanzania imepangwa kucheza mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza dhidi ya Kenya itakayofanyika kati ya Februari 13 na 15 mwaka huu jijini Mombasa. Mechi ya marudiano itachezwa wiki moja baadaye nchini.

Zanzibar imewasili na kikosi cha wachezaji 14 na viongozi watatu ambacho kitaungana na kile cha Tanzania Bara. Timu hizo zitacheza jumla ya mechi nane kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam.

Mechi hizo zitachezwa mbili asubuhi na mbili jioni kesho (Januari 24 mwaka huu), na nyingine nne kwa utaratibu huo huo keshokutwa (Januari 25 mwaka huu) kabla ya Kocha John Mwansasu kutaja kikosi cha mwisho Januari 26 mwaka huu.

VPL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 12 wikiendi hii kwa mechi saba. Kesho (Januari 24 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Polisi Morogoro na Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mechi za Jumapili ni kati ya Azam na Simba (Uwanja wa Taifa), Kagera Sugar na Ndanda (Uwanja wa CCM Kirumba), Stand United na Coastal Union (Uwanja wa Kambarage),, Mbeya City na Tanzania Prisons (Uwanja wa Sokoine), Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar (uwanja wa Mabatini), na JKT Ruvu na Mgambo Shooting (Uwanja wa Azam Complex).

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment