Thursday, 13 November 2014

KAMATI YA SHERIA YAPITISHA USAJILI SDL

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imepitisha usajili wa Ligi Daraja la Pili (SDL) huku ikikata majina mawili ya wachezaji katika klabu za Abajalo ya Dar es Salaam na Magereza ya Iringa.

Klabu hizo mbili zilisajili wachezaji 31 badala ya 30 ambapo ni kinyume na Kanuni ya 61(2) ya Ligi Daraja la Pili inayoruhusu klabu kusajili wachezaji wasiozidi 30 na wasiopungua 18.

Wachezaji ambao Kamati ya Sheria iliyokutana jana (Novemba 11 mwaka huu) imewaondoa ni wale waliokuwa wameorodheshwa namba 31 katika usajili wa klabu hizo. Wachezaji hao ni Andrew Mathew Kazembe (Abajalo) na Joshua Omari (Magereza).

Michuano ya Ligi Daraja la Pili inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.

Wachezaji waliopitishwa katika kila klabu na idadi yao kwenye mabano ni Abajalo (30), Arusha FC (18), Bulyanhulu (28), Kariakoo (30), Kiluvya United (23), Magereza (30), Mbao (27), Milambo (29), Mji Mkuu (29) na Mkamba Rangers (30).

Wengine ni Mpanda United (29), Mshikamano (28), Mvuvumwa (18), Njombe Mji (25), Pamba (24), Rwamkoma JKT (25), Singida United (26), Town Small Boys (22), Transit Camp (28), Ujenzi Rukwa (30), Volcano (25) na Wenda (20).

Klabu zote zinakumbushwa kulipia na kuchukua leseni za wachezaji wao kabla ya ligi kuanza, kwani kwa mujibu wa kanuni hakuna mchezaji atakayeruhusiwa kucheza mechi ya ligi bila kuonyesha leseni yake. 

WATANO WAUNDA JOPO KUHAKIKI UMRI COPA
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeunda jopo la watu watano kuhakiki umri wa wachezaji watakaoshiriki hatua ya ngazi ya Taifa ya michuano ya Copa Coca-Cola 2014.

Michuano hiyo ya ngazi ya Taifa itafanyika Dar es Salaam kuanzia Desemba 13 hadi 20 mwaka huu. Uhakiki wa umri utafanyika Desemba 11 na 12 mwaka huu wakati timu zote zinatakiwa kuwasili Shule ya Filbert Bayi mkoani Pwani kuanzia Desemba 10 mwaka huu.

Jopo hilo la uhakiki linaongozwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Henry Tandau. Wengine katika jopo hilo ni Ally Mayay, Charles Boniface Mkwasa, Dk. Jonas Tiboroha na Richard Yomba.

Timu 16 zitakazocheza michuano hiyo inayoshirikisha watoto wenye umri chini ya miaka 15 ni Arusha, Dodoma, Geita, Katavi, Kigoma, Kinondoni, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Lindi, Mbeya, Mjini Magharibi, Morogoro, Mwanza, Ruvuma, Simiyu na Tanga.

Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vinakumbushwa kutuma TFF fomu za usajili ambazo zinatakiwa kuambatanishwa vyeti vya kuzaliwa vya wachezaji husika.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment