Saturday, 29 November 2014

UFAFANUZI WA MASUALA MBALIMBALI YA TIMU YA MBEYA CITY COUNCIL FOOTBALL CLUB.

MBEYA CITY COUNCIL FOOTBALL CLUB


Klabu ya Mbeya City Council Football Club leo 25/11/2014 inatoa ufafanuzi wa mbalimbali ikiwemo suala la utaratibu wa maslahi kwa watumishi wake (benchi la ufundi, wachezaji na watumishi wengine) na uwepo wa fedha za wadhamini katika klabu yetu.

Uamuzi wa kutoa taarifa hii umefikiwa baada ya vikao vya menejimenti na kamati ya fedha na utawala kufuatia taarifa mbalimbali zinazozalishwa kila siku juu ya klabu yetu toka katika vyanzo ambavyo sio vya klabu

MASLAHI YA WACHEZAJI
Hivi karibuni baadhi ya wadau wa mchezo wa mpira wa miguu wamehusisha matokeo ya uwanjani iliyopata timu na maslahi kwa wafanyakazi wa klabu kama taasisi.

Sehemu kubwa ya wafanyakazi wa klabu ikijumuisha timu ni wafanyakazi chini ya masharti ya mkataba chini ya muajili ambaye ni Halmashauri ya jiji la Mbeya, Hivyo maslahi ya mfanyakazi(kwa kada hii) hujadiliwa na kukubaliana kwa pande zote mbili(Klabu kwa niaba ya muajiri na Mchezaji kama muajiriwa) kulingana na bei ya soko ndipo mkataba husainiwa.

Klabu imeweka utaratibu wa namna ya wafanyakazi wake kujadiliana na mwajili kuhusu mambo mbali mbali yenye lengo la kuboresha utendaji wa kazi na mazao yake pamoja na masuala ya maslahi pindi kukiwa na haja hiyo.

Mishahara ya wachezaji pamoja na kuamuliwa kwa makubaliano baada ya majadiliano ya pande zote mbili pia bei ya soko huangaliwa na kuzingatiwa. Msimu wa 2014/2015 mishahara ya wachezaji ilipanda kati ya asilimia 100 – 300(%) ikilinganishwa na msimu uliopita 2013/2014.

Posho zote zitolewazo na klabu zilirekebishwa ikilinganishwa na msimu uliopita kwa kuzingatia makubaliano kati ya wachezaji na menejimenti kabla ya kuanza kwa msimu huu.

Klabu inatambua wazi kuwa mpira ni ajira kama zilivyo ajira zingine,maslahi haya yamewekwa kwa makusudi ili kuboresha hali za maisha za wafanyakazi wetu hasa wachezaji kwani hiyo ndiyo ajira yao.
Ukiondoa mshahara unaoendelea kulipwa kila mwezi hakuna mfanyakazi yeyote anayedai chochote kati ya maslahi yake.

FEDHA ZA WADHAMINI:

Pamoja na kuwa na kipengele cha kutotoa siri (Confidentiality)za mikataba yetu na wadhamini wetu, klabu inasikitishwa namna ambavyo umma wa wanamichezo unavyopotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa changamoto ambazo klabu inapitia hivi sasa kama taasisi zinatokana na kuwepo kwa fedha za wadhamini.

Klabu inaomba ikumbukwe kuwa katika msimu uliopita 2013/2014 ilitumia zaidi ya shilingi milioni 700 kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri ikiwa kama mmiliki wa klabu. Wadhamini kwa mujibu wa makubaliano hawajatoa wala hawatoi fedha zote mara moja kwa mujibu wa mkataba, fedha hizo hutolewa kila mwezi na kwa awamu.

Matumizi ya kawaida ya klabu kwa mwezi si chini ya shilingi 49,000,000.00(bila kuhusisha mishahara), katika kipindi cha Julai-Sept 2014, Klabu ilikuwa na mdhamini mmoja tu ambaye ni Binslum tyres Co Ltd anayetoa shilingi 15,000,000.00 kwa mwezi sawa na shilingi 180,000,000.00 kwa mwaka kwa mujibu wa mkataba uliopo.

Ukiangalia mahitaji ya klabu kwa mwezi mmoja hapo juu, fedha hizi za mdhamini zilichangia asilimia 30.6(%) ya gharama za klabu kwa mwezi.  Hii ikiwa na maana kuwa bado asilimia 69.4(%) ya gharama za uendeshaji wa timu zilitoka Halmashauri.

Kuanzia mwezi oktoba 2014 ambapo kampuni ya coca cola ilisaini mkataba wa udhamini na klabu yetu. Kampuni ya Coca Cola itakuwa inatoa fedha taslimu Tsh 60 milioni ambazo inazitoa kwa mwaka. Fedha hizi hutolewa kila baada ya robo mwaka shilingi milioni 15. Hii ina maana kuwa coca cola inatoa shilingi 5,000,000.00 milioni kila mwezi.

Hivyo kuanzia mwezi oktoba klabu inapata toka kwa wadhamini wake wawili (Binslum Tyre Co Ltd na Coca Cola Kwanza) shilingi 20,000,000.00 kwa mwezi. Fedha hizi zinachangia asilimia 40.8(%) ya gharama za uendeshaji wa timu kwa mwezi na asilimia 59.2(%) ya gharama hizo bado zinabebwa na Halmashauri.

Uwepo wa wadhamini hivi sasa haujaongeza fedha kutoka katika bajeti hiyo bali umepunguza utegemezi wa timu kwa Halmashauri.
Hivyo basi shutuma zinazotolewa na baadhi ya wadau  kuwa changamoto ambazo timu inazipitia kwa sasa ni kutokana na kuwepo kwa fedha za wadhamini ni
UPOTOSHAJI MKUBWA.
MWALIMU JUMA MWAMBUSI

Mwalimu Juma Mwambusi ni muajiriwa wa Halmashauri ya jiji la Mbeya anayesimamia benchi la ufundi la timu yetu.

Menejiment ilikutana na Mwl Juma Mwambusi katika vikao vyake vya kawaida kupitia changamoto kadhaa zilizojitokeza katika michezo saba ya awali mara baada ya kuwasilisha ripoti ya maendeleo ya timu. Mwalimu Mwambusi na menejiment tumeridhiana kwa faida ya mpira wa miguu na jamii inayoizunguka timu yetu anaendelea kuifundisha timu ya Mbeya City Fc.

Nachukua nafasi hii kuujulisha umma kuwa Mwl.Juma Mwambusi ndiye Kocha Mkuu wa timu na hivi sasa anandaa program ya mafunzo kwa mzunguko wa pili wa ligi unaotarajia kuanza disemba 2014.

MWISHO

Klabu kama taasisi inayokuwa inapitia katika changamoto mbalimbali, ni imani ya menejimenti kuwa changamoto hizi zitaiimarisha na kuikomaza klabu ili kuwa klabu bora zaidi kwa vizazi vijavyo.

Tunatoa shukrani za dhati kwa wadau wetu wote wanaoendelea kutuunga mkono katika kipindi hiki.
Imetolewa na

E.E.Kimbe
KATIBU MKUU
MCC FC 

No comments:

Post a Comment