Alliance for Change and
Transparency-Tanzania
(Mabadiliko na Uwazi)
- Mnamo tarehe 11
Novemba 2014 kuliripotiwa na vyombo vya habari kwamba Katibu Mkuu wa
ACT-Tanzania Ndugu Samson Mwigamba alikuwa ‘ametimuliwa’ katika nafasi
yake na vijana waliojiita waasisi wa chama, ambao ni Ndugu Greyson
Nyakarungu na Ndugu Leopold Mahona. Tunakiri kwamba Ndugu Greyson
Nyakarungu na Ndugu Leopold Mahona ni wajumbe katika Kamati ya muda ya
Uongozi ya chama. Ndugu Leopold Mahona ni Naibu Katibu Mkuu (Bara) wakati
Ndugu Greyson Nyakarungu ni Mjumbe wa Kamati.
- Kwa utamaduni wa
chama cha ACT-Tanzania, tangazo la vijana hawa lilichukuliwa kama
kiashiria cha tatizo linalohitaji kutatuliwa, na ambalo lilielekea
kuchafua hali ya kisiasa na amani ndani ya chama. Kwa sababu hiyo, Kamati
ya Uongozi ilikutana kwa muda wa siku mbili Jijini Dar es Salaam na
kujadili kwa kina dukuduku walizokuwa nazo Ndugu Mahona na Ndugu
Nyakarungu.
- Kwa kuwa chama chetu
kinaamini katika uhuru kamili wa maoni ambayo yanaweza kutolewa kwa njia
mbalimbali ikiwemo mikutano na waandishi wa habari, Kamati ya Uongozi
ilipokea taarifa iliyosambazwa katika vyombo vya habari na Ndugu
Nyakarungu na Ndugu Mahona kwa tahadhari kubwa katika kulinda misingi ya
chama na haki ya viongozi na wanachama kutoa maoni yao chanya na hasi kwa
uwazi.
- Baada ya majadiliano
marefu na tafakuri ya kina, viongozi tumekubaliana:
- kujenga utamaduni wa
kuwasiliana mara kwa mara na tabia ya kutoa dukuduku zetu ndani ya vikao
vya chama
- Pale ambapo ni
muhimu kutumia vyombo vya habari kutoa dukuduku zetu kuhusu mwenendo wa
viongozi wenzetu ni vizuri kufanya hivyo katika namna ambayo italinda
misingi ya chama na kuendeleza udugu, umoja na amani ndani ya chama chetu
na jamii kwa ujumla.
- Tunatoa wito kwa
viongozi wetu na wanachama kwa ujumla kuendelea na maandalizi ya uchaguzi
wa serikali za mitaa. Tunawakikishia kwamba viongozi wenu
wote katika ngazi ya kitaifa tupo pamoja na tunaendelea kuchapa kazi kama
kawaida.
Kadawi Lucas Limbu, Mwenyekiti wa Taifa.
No comments:
Post a Comment