Monday, 17 November 2014

TFF YAIPONGEZA AFRIKA KUSINI KWA KUFUZU AFCON


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa pongezi kwa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kufuatia timu yake ya Taifa (Bafana Bafana) kufuzu kucheza fainali zijazo za AFCON nchini Equatorial Guinea.

Afrika Kusini iliifunga Sudan mabao 2-1, hivyo kufuzu kabla ya kukamilisha michezo yote. Bafana Bafana bado imebakiza mchezo mmoja katika hatua hiyo.

Wakati huo huo, TFF imeipeleka barua ya shukrani kwa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kwa kufanikisha kambi ya Taifa Stars nchini humo kabla ya kwenda kucheza Swaziland.

SAFA ilitoa viwanja vya mazoezi kwa Taifa Stars na usafiri wa basi la kisasa kutoka Johannesburg kwenda Swaziland na kurudi, hivyo kuokoa zaidi ya dola 15,000 ambazo TFF ingetumia kama ingegharamia yenyewe safari hiyo au kuweka kambi ya timu hiyo nyumbani.

Awali Benchi la Ufundi la Taifa Stars chini ya Kocha Mart Nooij lilipendekeza timu kufika Swaziland mapema au kuweka kambi nchini Afrika Kusini. SAFA ikajitolea kusaidia kambi hiyo.

Pia TFF inakanusha madai ya gazeti moja la kila siku lililodai kuwa wakaguzi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wamevamia/wamefanya ukaguzi wa siri kukagua fedha za udhamini wao kwa Taifa Stars.

Ukaguzi wa hesabu ni utaratibu wa kawaida wa kila robo ya mwaka wa fedha. TFF ndiyo huwaalika TBL kutuma wakaguzi wao ili kuhakiki vitabu vya fedha. Uhusiano kati ya TFF na TBL ni mzuri, na kila kinachofanyika ni kwa nia njema kwa makubaliano ya pande zote mbili.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment