Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu iliyokuwa ianze
kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu kwa mechi kumi katika viwanja vitano tofauti
imesogezwa mbele hadi Desemba 6 mwaka huu.
Mechi hizo zimesogezwa ili kutoa fursa ya kukamilisha maandalizi mbalimbali
ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Mikoa yenye timu katika ligi hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma,
Iringa, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa,
Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora.
MASHINDANO YA
TAIFA YA U12 YASOGEZWA
Mashindano ya Taifa kwa vijana wenye
umri chini ya miaka 12 yanayoshirikisha kombaini za mikoa yote ya Tanzania
yatafanyika jijini Mwanza kuanzia Desemba 30 mwaka huu hadi Januari 5 mwakani.
Awali mashindano hayo yalipangwa kuanza Desemba
6 mwaka huu, lakini yamelazimika kuyasogeza ili kutoa fursa ya kukamilika kwa matengenezo
ya viwanja vitatu ambayo vitatumika.
Kila timu ya mkoa inatakiwa kuwa na
ujumbe wa watu 16, wakiwemo wachezaji 14 na makocha wawili katika mashindano
hayo ya timu yenye wachezaji saba (7 aside).
Timu zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza
kuanzia Desemba 28 mwaka huu tayari kwa ajili ya uhakiki wa umri na taratibu
nyingine za mashindano. Timu zote zitafikia katika shule ya Alliance (Alliance
Schools).
Wachezaji wanaotakiwa kushiriki
mashindano hayo ni wenye umri chini ya miaka 12, hivyo ni wale waliozaliwa
kuanzia Januari 2003 na kuendelea.
RAMBIRAMBI
MSIBA WA MUNYUKU, KARASHANI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya waandishi wa
habari Innocent Munyuku na Baraka Karashani vilivyotokea jana (Novemba 19 mwaka
huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba
huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari nchini kwa
ujumla kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa mpira wa miguu
nchini kupitia kalamu zao.
Munyuku
alikuwa mmoja wa waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati Karashani
kwa nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo
kampuni ya New Habari 2006 akiripoti habari za mpira wa miguu.
Tunatoa
pole kwa familia za marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA), na kampuni ya New Habari 2006 na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment