WAZIRI wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Lazaro Nyalandu ametoa wito kwa Viongozi wa dini wote nchini kupaza
sauti kwa pamoja kukemea vitendo vya Ujangili pamoja na Uharibifu wa
mazingira nchini.
Wito huo ameutoa leo jijini Dar
es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa viongozi wa dini unaolenga
kuwaelimisha viongozi hao kutoa elimu kwa waumini wao juu ya kupinga
suala la ujangili na kuwasihi juu ya utunzaji wa mazingira.
Mhe. Nyalando alisema kuwa,
vitendo vya ujangili vikiendelea vinaweza kuleta athari kubwa nchini
ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na kuharibu sekta ya utalii
kwa Mbuga za wanyama.
“Serikali imeamua kwamba, mtu
yoyote anayefanya vitendo vya kijangili akijisalimisha na kukabidhi
silaha yake atasamehewa,” Alisema Mhe. Nyalando
Aliwasihi akina mama wanaojua waume zao wanaojihusisha na vitendo vya ujangili kuacha na kujisalimisha Wizarani.
Naye Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu
la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Alhaj Mussa Salum ameonyesha
ushirikiano na kuunga mkono utoaji wa elimu hiyo kwa waumini kwani hata
Quran Tukufu inahubiri juu ya haki za wanyama, hivyo ukatili juu ya
wanyama sio jambo zuri mbele za Mungu.
“Dhuluma inayofanyika kwa
wanyama ni dhambi kwani Quran inasema fanyeni wema kwani mwenyezi Mungu
anapenda wema” Alisema Sheikh Mussa.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo
la Iringa Baraza ka Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa alisema kuwa rasilimali zote zilizopo nchini ni Baraka,
hivyo zinapaswa kutunzwa na kuepuka suala la ubinafsi kwa kutaka
kuzitumia zote kwa haraka na kuzimaliza.
“Tufikirie na kizazi kijacho
kitahitaji kunufaika na rasilimali asilia hizi, mfano miti inayochukua
muda mrefu kuota pamoja wanyama wa porini”,alisema Askofu Ngalalekumtwa.
Naye mdau wa maendeleo nchini
Dkt. Regnald Mengi alisema kwamba, viongozi wa dini wana nguvu kubwa
katika jamii, kwani chochote wanachokisema kwa waumini wao ni rahisi kwa
waumini hao kukifuata kwani wanaamini chochote kinachosemwa nao ni
maagizo ya Mungu.
Mkutano huo ulihusisha viuongozi
mbalimbali wa kidini wakiwemo Maaskofu, Masheikh pamoja, Wadau wa
maendeleo wa UNDP pamoja na Mashirika mbalinmbali ya Wanyamapori
yakiwemo TANAPA, TAWIRI, FZC, AWF, WWF, ICCF ambao wenyeji wa mkutano
huo.
No comments:
Post a Comment