Friday, 6 June 2014

MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZINGIRA YATOA MSISITIZO WA USIMAMIZI WA SHERIA ZA UHIFADHI WA MAZINGIRA.

………………………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.Dar es salaam.
Serikali mkoa wa Dar es salaam imewataka watendaji wote wenye dhamana ya uhifadhi wa mazingira kulinda na kusimamia usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya jiji ili kufikia malengo ya kuwa na jiji safi na salama.
 Mkuu wa wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amesema kuwa suala la utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi na kusisitiza kuwa watendaji katika mamlaka mbalimbali za jiji la Dar es salaam wanalojukumu la kuhakikisha kuwa wanasimamia sheria zilizowekwa.
Amesema Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani  kuadhimisha  kilele cha wiki ya mazingira duniani kwa mwaka 2014 kwa ngazi ya mkoa na taifa kwa kueleza hatua zilizofikiwa katika uhifadhi wa mazingira na kueleza kuwa kitaifa  maadhimisho hayo yanafanyika  mkoani Mwanza chini ya Kauli Mbiu Tunza Mazingira ili Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema uongozi wa mkoa unaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha jiji la Dar es salaam linakuwa safi ikiwa ni pamoja na usimamizi wa sheria ndogo zinazohusiana na usafi na utunzaji wa mazingira kwa  kuwabana wanaochafua mazingira kwa kutupa ovyo,utiririshaji wa majitaka kwenye mitaro ya barabara, kuzuia uchimbaji wa mchanga,Vifusi na kokoto katika kingo za mito na maeneo yote yasiyo rasmi.
Hatua nyingine ni kudhibiti ujenzi holela katika maeneo yanayozuia mikondo ya maji mabondeni na kuzuia ufanyaji wa biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Bi. Mjema ameeleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokea sasa yanasababisha ongezeko la joto duniani,kuongezeka kwa kina cha bahari na kusababisha kumomonyoka na kuzama kwa fukwe za bahari,ongezeko la vipindi virefu vya ukame, ongezeko la mvua nyingi zaidi ya viwango vya kawaida hali inayosababisha mafuriko na kuambatana na milipuko ya magonjwa mbalimbali.
Kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu amesema kuwa inatoa chagizo kwa wananchi kuanzia mtu mmojammoja kutoa mchango katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kutoa wito kwa jamii kutathmini madhara yatokanayo ya shughuli za kibinadamu zinazoongeza hewa ya ukaa zikiwemo za uchomaji wa mkaa, misitu, moshi kutoka viwandani na kwenye magari na baadhi ya vifaa vya majumbani kama vile majokofu na viyoyozi.
“Mabadiliko ya tabia nchi yana athari kubwa sana katika mazingira yetu, wataalam wanatuambia kwamba njia ya asili ya kupunguza hewa ukaa angani ni kuwa na misitu,nasisitiza tuwe na utamaduni wa kupanda, kutunza na kuhifadhi misitu yetu kwani hunyonya hewa hiyo, hii ni sababu mojawapo inayonifanya kusisitiza suala la kupanda na kutunza miti” Amesema.
Aidha, ameeleza kuwa maadhimisho ya wiki ya mazingira mkoa wa Dar es salaam yalitanguliwa na shughuli mbalimbali zinazohamasisha utunzaji na usimamizi wa mazingira katika halmashauri za manispaa ya Kinondoni, Ilala na Temeke kuanzia tarehe 1 mpaka tarehe 5 mwezi huu.

No comments:

Post a Comment