Sunday, 15 June 2014

MAMA KIKWETE AITAKA JAMII KUJENGA TABIA YA KUCHANGIA DAMU KWA HIARI

Jamii imetakiwa kujenga tabia ya kuchangia damu kwa hiari kitendo ambacho kitapunguza  vifo vya kina mama wajawazito 363 vinavyotokea kila mwaka kutokana na tatizo la ukosefu wa damu wakati wa kujifungua.
Kauli  hiyo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi wa mkoa wa Kigoma kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wachangia damu Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani humo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema takwimu zinaonyesha kuwa takribani wanawake 454 kati ya vizazi hai laki moja hufa kila mwaka kutokana tatizo la uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa damu.
“Ni dhahiri vifo vinavyotokana na uzazi viko juu na kwa bahati mbaya waathirika wakubwa ni wasichana chini ya umri wa miaka 15, makundi mengine yanayohitaji kuongezewa damu ni kina mama wajawazito wakati wa mimba na kujifungua , watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa ukosefu wa damu unaosababishwa na malaria kali na magonjwa mengine, ajali, wagonjwa wa saratani, upasuaji mkubwa wa moyo, anemia, seli mundu na hemophilia.
Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kwamba tunatoa damu ili jamii yetu iweze kutimiza mahitaji yake kwani tunapokuwa na akiba ya damu iliyo salama tunajihakikishia tiba ya ndugu zetu pale wanapopata matatizo bila ya siye kulazimika kutoa damu ya papo kwa hapo”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti hiyo wa WAMA alisema mtu yeyote mwanamke au mwanaume anaweza kuchangia damu ikiwa ana afya njema, umri kati ya miaka 18 hadi 65, uzito usiopungua kilo 50, uwingi wa damu zaidi ya gramu 12 kwa desilita, kutokuwa na shinikizo la damu na  kwa mwanamke asiwe mjamzito au ananyonyesha.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii  Dkt. Stephen Kebwe alisema tangu kuanzishwa kwa mpango wa damu salama mwaka 2004 kumekuwa na ongezeko la wachangia damu kwa hiari kutoka kiasi cha chupa 5000 kwa mwaka 2005 hadi chupa 160000 kwa mwaka 2013.
“Changamoto zinazoukabili mpango huu ni mahitaji makubwa kuliko upatikanaji wa damu inakadiriwa  mahitaji ya damu kwa mwaka kitaifa ni wastani wa  chupa 400000 hadi 450000, uelewa mdogo wa jamii kuhusu suala zima la uchangiaji damu kwa hiari, uuzwaji wa damu usio halali Hospitalini jambo ambalo linakatisha tamaa wachangia damu wa hiari na matumizi yasiyo sahihi ya damu katika Hospitali”, alisema Dkt. Kebwe.
Naibu waziri huyo wa Afya na Ustawi wa Jamii alisema mpango wa taifa wa damu salama unaendelea kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji wa damu katika jamii, kuendelea kujenga vituo vidogo vya kuchangia damu,  kutoa majibu, nasaha, na malezi kwa wiki mbili mpaka nne baada ya mtu kuchangia damu na kuongeza mazao mbalimbali ya damu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issah Machibya aliwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kujitoa kwao katika zoezi zima la uchangiaji wa damu salama na kuweza kukusanya chupa 3620 kwa kipindi cha wiki tatu  kabla ya kilele cha maadhimisho hayo na hivyo kuvuka malengo kwa asilimia 121 kwani kabla ya kuanza kwa zoezi hilo walijipangia kukusanya chupa salama za damu 3000

No comments:

Post a Comment